Wednesday, February 24, 2010

UKAGUZI WA MAZINGIRA YA CHANZO CHA MAJI NJORO YA GOA

Mkaguzi wa mazingira kutoka Manispaa ya Moshi akiandika alama za maoni yake juu ya chanzo cha maji cha asili cha Njoro ya Goa.
Wakulima na wakaguzi wa mazingira wakijadiliana.

Wakaguzi wa mazingira wakiweka alama katika makabrasha yao.



Saturday, February 20, 2010

MKUU WA MKOA KILIMANJARO AFURAHIA UTENDAJI KAZI ZA KILIMO - KATA YA KALOLENI

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mama Monica Mbega (MB) hapa anajiandaa kupokea zawadi ya mchele kutoka kwa wakulima ili naye ajisikie kwa kile wakulima wanachozalisha katika skimu ya umwagiliaji Kaloleni.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, mama Monica Mbega akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Mtendaji wa kata ya Kaloleni pamoja na baadhi ya wanakamati wa ukarabati mifereji kaloleni huku akiangalia mfereji uliojengwa kwa mawe katika skimu ya Kaloleni, eneo la Njoro ya Goa.

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, mama Monica Mbega akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika mashamba ya Skimu ya umwagiliaji, Njoro ya Goa.



MKUU WA MKOA AKIWA KALOLENI

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, akipata maelezo kutoka kwa mwakilishi wa Vijana wapanda mlima "Mount Kilimanjaro Porters Society" ambao wanashirikiana na wakulima katika kuboresha chanzo cha maji cha Goa.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Kaloleni akimwongoza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Monica Mbega kukagua mashamba ya mpunga huku akiongozana na wakulima.


Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro akisaini kitabu cha wageni alipowasili mashamba ya Mpunga Skimu ya umwagiliaji Kaloleni katika eneo la Njoro ya Goa.


Friday, February 19, 2010

ZIARA YA MKUU WA MKOA KILIMANJARO KUZUNGUMZA NA WAKULIMA WA MPUNGA

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi wakikagua mashamba ya umwagiliaji mpunga katika skimu ya Kaloleni.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa mbele ya wakulima.




Wakulima wakati wakimsubiri Mkuu wa Mkoa awasili.


Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro alifika katika Kata ya Kaloleni akiongozana na viongozi mbalimbali wa Mkoa pamoja na Wilaya katika kukagua shughuli za kiserikali zinazoendelea katika Kata ya Kaloleni. Katika ziara yake alitembelea wakulima wa skimu ya mpunga ili kujionea mwenyewe jinsi miradi ya kilimo hususan ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji inavyofanywa.


PIa alipata wasaa wa kuzungumza na wakulima na kupokea taarifa ya utendaji kazi ya Kata kwa upande wa masuala ya kilimo
.

MKUU WA MKOA ATEMBELEA KALOLENI

Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Bi. Bernadete Kinabo, akizungumza na wakulima Kaloleni
Mkuu wa Mkoa akizungumza na baadhi ya wakulima wa Skimu ya Umwagiliaji ya Kaloleni alipowatembelea wakulima hao.


Bi. Klimo wa Kata ya Kaloleni , Bi. Mariam Muya, akisoma taarifa ya utendaji kazi ya idara ya Kilimo na Mifugo ya Kata kwa Mkuu wa Mkoa huko mashambani Njoro ya Goa.

TAARIFA HIYO HII HAPA CHINI

TAARIFA YA UTENDAJI KAZI IDARA YA KILIMO – KATA YA KALOLENI KWA MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO MHESHIMIWA MONICA MBEGA (MBUNGE) 18/02/2010

UTANGULIZI

Awali ya yote, nikukaribishe wewe binafsi pamoja na ujumbe wako katika skimu Kilimo cha umwagiliaji ya Kaloleni. Tukiwa kama wadau wakuu wa kilimo tunafarijika sana kujiwa na ugeni mkubwa kama wa leo. Taarifa hii inazingatia utekelezaji wa programu mbalimbali za kilimo zinazofanyika katika Kata ya Kaloleni hususan katika Skimu ya Kaloleni.

Skimu ya Kaloleni ina ukubwa wa kadiri hekta mia moja kumi na nane (118) na inaendesha kilimo cha mpunga kwa kujumuisha wakulima wadogowadogo wapatao mia nne na sabini (470). Wakulima wanaolima katika Skimu hii ni wakazi wa Kata ya Kaloleni na Pasua. Shughuli za kilimo hapa zinaendeshwa na wenye mashamba / vieneo vidogo vidogo na wakulima wengine wanakodisha.

Skimu hii imegawanyika katika maeneo makuu mawili ambapo wakulima wanaendesha kilimo chao kwa kutegemea maji kutoka katika vyanzo vya maji vya kiasili vilivyomo hapahapa. Eneo la kwanza linaitwa Njoro ya Goa upande wa magharibi na Njoro ya Liwali upande wa mashariki. Katika maeneo yote mawili, wakulima wana uongozi ambao ndio unaotegemewa katika kuratibu shughuli mbalimbali zenye kuwezesha maendeleo ya Skimu hii. Shughuli ambazo serikali kupitia Halmashauri ya Manispaa inazisimamia na kuzitolea muongozo ni kama ifuatavyo:

A: UJENZI WA MIFEREJI

1. MFEREJI NAMBA MOJA – NJORO YA GOA
Napenda kukutaarifu kuwa wakulima wa skimu hii wana ushirikiano mzuri na wa karibu katika kushirikishwa utekelezaji wa programu mbalimbali za serikali zenye kuwagusa wakulima moja kwa moja. Kwa mfano, tayari Halmashauri ya Manispaa kupitia idara ya Kilimo imeimarisha miundo mbinu ya umwagiliaji kwa kujenga mfereji wenye urefu wa meta 1450 katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2008 -2009.

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,

Mwezi July 2008 katika kuwawezesha wakulima wa Mpunga kiumwagiliaji, serikali kupitia Mpango wa Kuendeleza Kilimo wa Wilaya (District Agricultural Development Program – DADP) ilitoa shilingi Milioni ishirini na mbili, laki tatu na themanini na saba elfu na sitini na tano (22,387,065/= ) kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa ajili ya Ujenzi wa Mfereji huo .Mradi huo umewashirikisha wakulima kama wasimamizi kupitia Kamati ya Usimamizi ya Wakulima wenyewe na ulilenga kujenga mfereji kwa slabs na baadhi ya sehemu kwa mawe. Hii ilijumuisha kuweka mikanda ya mfereji na pia kujenga vizuizi vya maji na vitolea maji kwenda sehemu mbalimbali za mashamba.

Mradi ulianza kutekelezwa na Kampuni ya Powerpoint Construction rasmi tarehe 08/10/2008 katika awamu ya kwanza kwa Mkandarasi kuchimba mitaro na baadaye kujengea slab hadi umbali wa meta 300. Hadi hatua hiyo zilitumika shilingi Milioni saba, laki tisa na themanini na tisa elfu na mia tano (7,989,500/=) kwa kazi hiyo ambayo ni asilimia 30%.

Kazi hiyo ilisimama mwezi December 2008 baada ya kutokea matatizo ya kiutekelezaji ya Mkandarasi, Mkandarasi alijitoa. Hata hivyo mkandarasi jamii alipewa kazi hiyo na amewezesha ujenzi wa mfereji kukamilika kwa meta 1450. Kwa sasa mfereji huo Namba moja Njoro ya Goa umerahisisha sana umwagiliaji na kudhibiti ugombeaji maji miongoni mwa wakulima pamoja na kuongeza kwa kiasi kikubwa cha maji mashambani.

2. MFEREJI NAMBA MOJA NJORO YA LIWALI

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,

Sio mfereji wa Njoro ya Goa tu, pia, mwishoni mwa mwaka jana (2009), Halmashauri ya Manispaa imeleta fedha kiasi cha shilingi milioni 25 ili kuendeleza ujenzi wa mifereji kupitia mpango wa DADP. Kwa sasa ujenzi umeanza mapema mwezi huu na unajengwa mfereji kwa mawe eneo la Njoro ya Liwali kuwawezesha wakulima wa eneo hilo kurahisisha umwagiliaji. Katika kazi hiyo, Kamati maalum ya Ukarabati wa mifereji ndiyo inayosimamia kazi hiyo kwa mwongozo wa kitaalam kutoka Idara ya Uhandisi Halmashauri ya Manispaa.

B: KILIMO KWANZA

Ukiacha suala la mifereji, pia tayari wakulima wametaarifiwa kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imetenga fedha, shilling Milioni 10, kwa ajili ya kuwanunulia wakulima wa Kaloleni matrekta madogo “power tillers” mbili kwa kuanzia katika kuwawezesha kupitia harakati za “Kilimo Kwanza”. Tunatarajia wakati wowote matrekta hayo kuwasili na utaratibu unaandaliwa jinsi gani matrekta hayo yatasimamiwa kwa kuwashirikisha wakulima wenyewe.

Kwa sasa wakulima wako katika mchakato wa kujipanga kimakundi ili kuwa na utaratibu utakaowezesha matumizi ya matrekta hayo uwe endelevu. Napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru serikali kwa mambo yote mazuri ambayo inafanya katika kumjali mkulima hasa wale wadogo kama wanaolima eneo kama la kwetu.

3. VOCHA ZA RUZUKU YA PEMBEJEO

Napenda nikujulishe kuwa wakulima wa Kaloleni tayari wamefaidika na zoezi la serikali la ugawaji wa vocha za ruzuku za pembejeo. Zoezi hili limeshatekelezwa hapa kwetu tangu mwaka jana ambapo hadi sasa wakulima wamekwishagawiwa vocha migao mitano (5) tangu mwaka jana 2009 – February hadi hata leo hii zoezi hili linaendelea kwa mara ya tano.

Kwa kupitia taarifa ya Kamati ya vocha ya wakulima wa Kaloleni, hadi zoezi la ugawaji vocha litakapokamilika mwishoni mwa wiki hii, wakulima wa Kaloleni watakuwa wamepewa jumla ya vocha elfu saba na ishirini na tano (7025) zikiwa ni vocha za mbolea za aina tatu: yaani kupandia na kukuzia zikijumuisha mbolea aina ya UREA, DAP na MINJINGU. Kimahesabu ni kuwa kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita, wakulima wa Kaloleni wamegawiwa vocha zenye thamani ya shilingi milioni mia moja sabini na tisa elfu, laki saba na sabini na mbili elfu (179,772,000/=) huu ni msaada mkubwa sana wa serikali kwa wakulima na tunaishukuru sana serikali kwa juhudi zake ambazo kwetu tunajivunia.


4. MAFUNZO KWA WAKULIMA

Wakulima wa Skimu ya Kaloleni wanapenda kumshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa kwa kufadhili mafunzo ya wakulima katika vipindi tofauti. Napenda nikutaarifu tu kuwa, katika kuhakikisha Kilimo cha kisasa kinafikiwa, mwaka 2008, wakulima wapatao 21 wa mpunga Kaloleni walihudhuria mafunzo ya kilimo hicho yaliyofanyika katika Chuo cha Kilimo – KATC. Katika mafunzo hayo, walijifunza mbinu za kisasa za kilimo cha mpunga na wakulima hao ambao walihudhuria mafunzo wamekuwa chachu kwa wenzao kuhimiza Kilimo cha kisasa. Mafunzo haya yaligharimiwa na Halmashauri ya Manispaa kwa kulipa shilingi milioni sita (6000000/=)

Tayari wakulima wanajua kuwa mwaka huu, 2010, mipango imeanza ya wakulima wapatao kumi (10) watahudhuria mafunzo katika chuo cha KATC kujifunza zaidi mbinu bora za kilimo cha mpunga.

5. UTUNZAJI VYANZO VYA MAJI

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,

Wakulima wa Kaloleni hawako nyuma katika suala la uboreshaji na utunzaji wa vyanzo vya maji. Napenda nikufahamishe kuwa kilimo katika skimu hii kinategemea maji ya chemichemi na ni wajibu wetu wakulima kutunza vyanzo hivyo vya maji. Kwa mantiki hiyo, ili kuhakikisha kuwa wakulima wa mpunga Kaloleni wanavitunza vyanzo vya maji, kwa kushirikiana na wadau binafsi, vijana wapanda mlima “Kilimanjaro Porters Society”, wameweza kupanda miti ipatayo elfu tatu (3000) katika kukilinda chanzo cha maji cha Goa. Chanzo hiki kinatoa maji ya umwagiliaji kwa wakulima wapatao mia tatu (300).

Pia pindi msimu wa mvua utakapoanza, tunatarajia mwezi Machi miti mingine elfu tano (5000) itapandwa kwa kuhakikisha kuwa hifadhi yote ya chanzo hicho inakuwa ni msitu. Wakulima tunatoa rai kwa serikali na hasa Halmashauri ya Manispaa, kutusaidia kwa ushauri na hata kama inawezekana tuweke uzio kuzunguka chanzo cha maji cha Njoro ya Goa.

TAMATI

Kwa ufupi hayo ndiyo mambo machache ambayo yanafanyika katika Skimu hii kwa kuzingatia utekelezaji wa program mbalimbali za serikali katika kuwasaidia wakulima wafikie malengo yao. Kwa niaba ya wakulima wa Skimu ya Kaloleni ninakushukuru sana kwa kututembelea siku yao leo. Tunaamini kuwa kuja kwako Kaloleni ni ishara kuwa serikali inajali wanakaloleni hususan wakulima wa skimu hii.

Kwa niaba ya wakulima wote wa skimu ya Kaloleni, nakutakia wewe pamoja na ujumbe wako maisha na afya njema.


Imeandaliwa na:

Mariam Muya
Bibi Kilimo- Kata ya Kaloleni